Home |  | Audio |  | Index |  | Verses

Mwanzo

Chapter: 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31 32 33 34 35 36 37 38 39 40 41 42 43 44 45 46 47 48 49 50

1 Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja.
2 Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko.
3 Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.
4 Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.
5 Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.
6 Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya.
7 Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.
8 Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.
9 Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote.
10 Hivi ndivyo vizazi vya Shemu; Shemu alikuwa mtu wa miaka mia akamzaa Arfaksadi miaka miwili baada ya gharika.
11 Shemu akaishi baada ya kumzaa Arfaksadi miaka mia tano, akazaa wana, waume na wake.
12 Arfaksadi akaishi miaka thelathini na mitano, akamzaa Sela.
13 Arfaksadi akaishi baada ya kumzaa Sela miaka mia nne na mitatu, akazaa wana, waume na wake.
14 Sela akaishi miaka thelathini, akamzaa Eberi.
15 Sela akaishi baada ya kumzaa Eberi miaka mia nne na mitatu, akazaa wana, waume na wake.
16 Eberi akaishi miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi.
17 Eberi akaishi baada ya kumzaa Pelegi miaka mia nne na thelathini, akazaa wana, waume na wake.
18 Pelegi akaishi miaka thelathini, akamzaa Reu.
19 Pelegi akaishi baada ya kumzaa Reu miaka mia mbili na kenda, akazaa wana, waume na wake.
20 Reu akaishi miaka thelathini na miwili, akamzaa Serugi.
21 Reu akaishi baada ya kumzaa Serugi miaka mia mbili na saba, akazaa wana, waume na wake.
22 Serugi akaishi miaka thelathini, akamzaa Nahori.
23 Serugi akaishi baada ya kumzaa Nahori miaka mia mbili, akazaa wana, waume na wake.
24 Nahori akaishi miaka ishirini na kenda, akamzaa Tera.
25 Nahori akaishi baada ya kumzaa Tera miaka mia na kumi na kenda, akazaa wana, waume na wake.
26 Tera akaishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani.
27 Na hivi ndivyo vizazi vya Tera. Tera akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani. Harani akamzaa Lutu.
28 Harani akafa kabla ya baba yake Tera katika nchi aliyozaliwa, yaani, katika Uru wa Wakaldayo.
29 Abramu na Nahori wakajitwalia wake. Jina la mkewe Abramu aliitwa Sarai, na jina la mkewe Nahori aliitwa Milka, binti Harani, ambaye alikuwa baba wa Milka na wa Iska.
30 Na Sarai alikuwa tasa, hakuwa na mtoto.
31 Tera akamtwaa Abramu mwanawe, na Lutu mwana wa Harani, mwana wa mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka wote katika Uru wa Wakaldayo, waende nchi ya Kanaani, wakafika mpaka Harani wakakaa huko.
32 Siku za Tera zilikuwa miaka mia mbili na mitano; Tera akafa katika Harani.

Top |  Next Chapter | Index |  | Home 
Full online version here [with search engine, multilingual display and audio Bible]