Mambo ya Walawi
1 Na mtu awaye yote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe;
2 au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, kama ni mzoga wa mnyama wa nyikani aliye najisi, au kama ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au kama ni mzoga wa mdudu aliye najisi, naye jambo hilo linamfichamania, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake;
3 au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu uwao wote ambao kwa huo amepata unajisi, na jambo hilo linamfichamania, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia;
4 au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo;
5 kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa;
6 naye atamletea Bwana sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake.
7 Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea Bwana hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa.
8 Naye atawaleta kwa kuhani, atakayemsongeza kwanza yule wa sadaka ya dhambi, naye atamkongonyoa kichwa shingoni mwake, lakini asimpasue vipande viwili;
9 kisha baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi atainyunyiza katika ubavu wa madhabahu; na damu iliyosalia itachuruzishwa hapo chini ya madhabahu; ni sadaka ya dhambi.
10 Kisha huyo ndege wa pili atamsongeza kuwa sadaka ya kuteketezwa, sawasawa na sheria; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.
11 Lakini asipowaweza hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, ndipo hapo atakapoleta matoleo yake kwa ajili ya neno hilo alilolikosa, sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, kuwa sadaka yake ya dhambi; asitie mafuta juu yake, wala ubani usitiwe juu yake; maana, ni sadaka ya dhambi.
12 Naye atamletea kuhani, na kuhani atatwaa konzi yake ya huo unga kuwa ukumbusho wake, na kuuteketeza juu ya madhabahu, juu ya sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto; ni sadaka ya dhambi.
13 Na huyo kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake ambayo katika mambo hayo mojawapo amefanya dhambi, naye atasamehewa; na unga uliosalia utakuwa wa kuhani, kama hiyo sadaka ya unga ilivyokuwa.
14 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
15 Mtu awaye yote akiasi na kufanya dhambi naye hakukusudia, katika mambo matakatifu ya Bwana; ndipo atakapomletea Bwana sadaka yake ya hatia, kondoo mume mkamilifu katika kundi lake; sawasawa na hesabu utakayomwandikia katika shekeli za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu, kuwa sadaka ya hatia;
16 naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa.
17 Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake.
18 Naye ataleta kondoo mume wa kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, amsongeze kwa huyo kuhani; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya jambo hilo alilolikosa pasipo kukusudia, asilijue, naye atasamehewa.
19 Ni sadaka ya hatia; hakika yake ni mwenye hatia mbele za Bwana.