1 Mambo ya Nyakati
1 Basi Daudi alikuwa mzee, ameshiba siku; akamtawaza mwanawe Sulemani awe mfalme juu ya Israeli.
2 Akawakusanya wakuu wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi.
3 Nao wakahesabiwa Walawi wenye miaka thelathini na zaidi; na jumla yao kwa vichwa, mtu kwa mtu, ikapata thelathini na nane elfu.
4 Katika hao ishirini na nne elfu walikuwa wa kusimamia kazi ya nyumba ya Bwana; na sita elfu walikuwa maakida na makadhi;
5 na elfu nne walikuwa mabawabu; na elfu nne walimsifu Bwana kwa vinanda, nilivyovifanya, alisema Daudi, vya kumsifia.
6 Basi Daudi akawagawanya kuwa zamu zao sawasawa na wana wa Lawi; Gershoni, Kohathi, na Merari.
7 Wa Wagershoni; Ladani, na Shimei.
8 Wana wa Ladani; Yehieli mkuu wao, na Zethamu, na Yoeli, watu watatu.
9 Wana wa Shimei; Shelomothi, na Hazieli, na Harani, watatu. Hao walikuwa vichwa vya mbari za baba za Ladani.
10 Na wana wa Shimei; Yahathi, na Zina, na Yeushi, na Beria. Hao wanne walikuwa wana wa Shimei.
11 Naye Yahathi alikuwa mkubwa wao, na Zina alikuwa wa pili; lakini Yeushi na Beria hawakuwa na wana wengi; basi wakawa mbari ya baba kwa kuhesabiwa pamoja.
12 Wana wa Kohathi; Amramu, Ishari, Hebroni, na Uzieli, watu wanne.
13 Wana wa Amramu; Haruni na Musa; naye Haruni akatengwa, ili ayatakase yaliyo matakatifu sana, yeye na wanawe milele, ili kufukiza uvumba mbele za Bwana, kumtumikia, na kubariki kwa jina lake, milele.
14 Lakini kwa habari za Musa, mtu wa Mungu, wanawe hutajwa miongoni mwa kabila ya Lawi.
15 Wana wa Musa; Gershomu na Eliezeri.
16 Wana wa Gershomu; Shebueli mkuu wao.
17 Na wana wa Eliezeri; Rehabia mkuu wao. Yeye Eliezeri hakuwa na wana wengine; lakini wana wa Rehabia walikuwa wengi sana.
18 Wana wa Ishari; Shelomithi mkuu wao.
19 Wana wa Hebroni; Yeria mkuu wao, Amaria wa pili, Yahazieli wa tatu, na Yekameamu wa nne.
20 Wana wa Uzieli; Mika mkuu wao, na Ishia wa pili.
21 Wana wa Merari; Mali na Mushi. Wana wa Mali; Eleazari, na Kishi.
22 Akafa Eleazari, wala hakuwa na wana, ila binti tu; na ndugu zao, wana wa Kishi, wakawaoa.
23 Wana wa Mushi; Mali, na Ederi, na Yeremothi, watu watatu.
24 Hao walikuwa wana wa Lawi, kwa kufuata mbari za baba zao, yaani, vichwa vya mbari za baba zao waliohesabiwa, kwa hiyo hesabu ya majina yao kwa vichwa, hao walioifanya kazi ya utumishi wa nyumba ya Bwana, wenye miaka ishirini na zaidi.
25 Kwa kuwa Daudi alisema, Bwana, Mungu wa Israeli, amewastarehesha watu wake; naye hukaa Yerusalemu milele;
26 wala Walawi hawahitaji tena kuichukua maskani, na vyombo vyake vyote kwa utumishi wake.
27 Maana kwa maneno ya mwisho ya Daudi, hao wana wa Lawi walihesabiwa, wenye miaka ishirini na zaidi.
28 Kwani kazi yao ilikuwa kuwangojea wana wa Haruni katika utumishi wa nyumba ya Bwana, nyuani, na vyumbani, na kwa kuvisafisha vitakatifu vyote, ndiyo kazi ya utumishi wa nyumba ya Mungu;
29 tena kazi ya mikate ya wonyesho, na ya unga mwembamba wa sadaka ya unga; ikiwa ni wa maandazi yasiyochachwa, au wa yale yaliyotokoswa, au wa yale yaliyookwa; na kazi ya kila namna ya kipimo na cheo;
30 nao wasimame kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Bwana, na jioni vivyo hivyo;
31 na kumtolea Bwana sadaka zote za kuteketezwa, katika siku za sabato, za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa, kwa hesabu kadiri ya agizo lake, daima mbele za Bwana;
32 tena walinde ulinzi wa hema ya kukutania, na ulinzi wa patakatifu, na ulinzi wa wana wa Haruni, ndugu zao, katika utumishi wa nyumba ya Bwana.