Zaburi
1 Haleluya. Mshukuruni Bwana,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake.
2 Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.
3 Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
4 Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote.
5 Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya, Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.
6 Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7 Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake.
8 Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
9 Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka.
10 Alilomthibitishia Yakobo liwe amri, Na Israeli liwe agano la milele.
11 Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa.
12 Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa, Naam, watu wachache na wageni ndani yake,
13 Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine.
14 Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.
15 Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.
16 Akaiita njaa iijilie nchi, Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
17 Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani.
18 Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.
19 Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya Bwana ilimjaribu.
20 Mfalme alituma watu akamfungua, Mkuu wa watu akamwachia.
21 Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake, Na mwenye amri juu ya mali zake zote.
22 Awafunge masheki wake kama apendavyo, Na kuwafundisha wazee wake hekima.
23 Israeli naye akaingia Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.
24 Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao.
25 Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake.
26 Akamtuma Musa, mtumishi wake, Na Haruni ambaye amemchagua.
27 Akaweka mambo ya ishara zake kati yao, Na miujiza katika nchi ya Hamu.
28 Alituma giza, kukafunga giza, Wala hawakuyaasi maneno yake.
29 Aliyageuza maji yao yakawa damu, Akawafisha samaki wao.
30 Nchi yao ilijaa vyura, Vyumbani mwa wafalme wao.
31 Alisema, kukaja makundi ya mainzi, Na chawa mipakani mwao mwote.
32 Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe, Na moto wa miali katika nchi yao.
33 Akaipiga mizabibu yao na mitini yao, Akaivunja miti ya mipaka yao.
34 Alisema, kukaja nzige, Na tunutu wasiohesabika;
35 Wakaila miche yote ya nchi yao, Wakayala matunda ya ardhi yao.
36 Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi, Malimbuko ya nguvu zao.
37 Akawatoa hali wana fedha na dhahabu, Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa.
38 Misri ilifurahi walipoondoka, Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia.
39 Alitandaza wingu liwe funiko, Na moto utoe nuru usiku.
40 Walipotaka akaleta kware, Akawashibisha chakula cha mbinguni.
41 Akaufunua mwamba, kukabubujika maji, Yakapita pakavuni kama mto.
42 Maana alilikumbuka neno lake takatifu, Na Ibrahimu, mtumishi wake.
43 Akawatoa watu wake kwa shangwe, Na wateule wake kwa nyimbo za furaha.
44 Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu;
45 Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake. Haleluya.