Home
| |
Audio
| |
Index
| |
Verses
Maombolezo
Chapter:
1
2
3
4
5
1
Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu.
2
Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.
3
Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4
Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.
5
Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.
6
Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7
Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8
Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9
Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10
Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.
11
Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni; Na mabikira katika miji ya Yuda.
12
Wakuu hutungikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13
Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14
Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani.
15
Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16
Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17
Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18
Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake.
19
Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20
Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi?
21
Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22
Isipokuwa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.
Top
| |
Next Chapter
| |
Index
| |
Home
Full online version
here
[with search engine, multilingual display and audio Bible]