1 Wakorintho
1 Je! Mimi si huru? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Ninyi si kazi yangu katika Bwana?
2 Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana ninyi ndinyi muhuri ya utume wangu katika Bwana.
3 Hilo ndilo jawabu langu kwa wale wanaoniuliza.
4 Je! Hatuna uwezo wa kula na kunywa?
5 Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?
6 Au je! Ni mimi peke yangu na Barnaba tusio na uwezo wa kutokufanya kazi?
7 Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi?
8 Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo?
9 Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe?
10 Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake.
11 Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?
12 Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo.
13 Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu?
14 Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.
15 Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu.
16 Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!
17 Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.
18 Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
19 Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi.
20 Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.
21 Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria.
22 Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.
23 Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.
24 Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.
25 Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.
26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;
27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.