Home |  | Audio |  | Index |  | Verses

Ayubu

Chapter: 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31 32 33 34 35 36 37 38 39 40 41 42

1 Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanyia mzaha, Ambao baba zao niliwadharau hata kuwaweka na mbwa wa kundi langu.
2 Naam, uwezo wa mikono yao utanifaa nini? Watu ambao nguvu zao zimekoma.
3 Wamekonda kwa uhitaji na njaa; Huguguna nchi kavu, penye giza la ukiwa na uharibifu.
4 Hung'oa mboga ya chumvi kwenye kichaka; Na mizizi ya mretemu ni chakula chao.
5 Hufukuzwa watoke kati ya watu; Huwapigia kelele kama kumpigia mwivi.
6 Lazima hukaa katika mianya ya mabonde, Katika mashimo ya nchi na ya majabali.
7 Hulia kama punda vichakani; Hukusanyika chini ya upupu.
8 Wao ni wana wa wapumbavu, naam, watoto wa wahuni; Walifukuzwa kwa mijeledi watoke katika nchi.
9 Na sasa mimi nimekuwa wimbo wao, Naam, nimekuwa simo kwao.
10 Wao hunichukia, na kujitenga nami, Hawaachi kunitemea mate usoni.
11 Kwani ameilegeza kamba yake, na kunitesa, Wala hawajizuii tena mbele yangu.
12 Kwa mkono wangu wa kuume huinuka kundi; Huisukuma miguu yangu kando, Na kunipandishia njia zao za uharibifu.
13 Waiharibu njia yangu, Wauzidisha msiba wangu, Watu wasio na msaidizi.
14 Wanijilia kama wapitao katika ufa mpana; Katikati ya magofu wanishambulia.
15 Vitisho vimenigeukia; Huifukuza heshima yangu kama upepo; Na kufanikiwa kwangu kumepita kama wingu.
16 Sasa nafsi yangu inamwagika ndani yangu; Siku za mateso zimenishika.
17 Wakati wa usiku mifupa yangu huchomeka ndani yangu, Na maumivu yanayonitafuna hayapumziki.
18 Kwa ugonjwa wangu kuwa na nguvu nyingi Mavazi yangu yameharibika; Hunikaza kama shingo ya kanzu yangu.
19 Yeye amenibwaga topeni, Nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
20 Nakulilia wewe, wala huniitikii; Nasimama, nawe wanitazama tu.
21 Wewe umegeuka kuwa mkali kwangu; Nawe waniudhi kwa uweza wa mkono wako.
22 Waniinua juu hata upeponi, na kunipandisha juu yake; Nawe waniyeyusha katika dhoruba.
23 Kwani najua kuwa utanileta hata kifoni, Niifikilie nyumba waliyoandikiwa wenye uhai wote.
24 Je! Mtu katika kuanguka kwake hanyoshi mkono? Na kulilia msaada katika msiba wake?
25 Je! Mimi sikulia kwa ajili ya huyo aliyekuwa katika taabu? Nafsi yangu, je! Haikusononeka kwa ajili ya wahitaji?
26 Hapo nilipotazamia mema, ndipo yakaja mabaya; Nami nilipongojea mwanga, likaja giza.
27 Matumbo yangu yatokota, wala hayaachi; Siku za taabu zimenijilia.
28 Naenda nikiomboleza pasipo jua; Nasimama katika mkutano, na kuulilia msaada.
29 Mimi ni ndugu yao mbwa-mwitu, Ni mwenzao mbuni.
30 Ngozi yangu ni nyeusi, nayo yanitoka, Na mifupa yangu imeteketea kwa hari.
31 Kwa hiyo kinanda changu kimegeuzwa kuwa maombolezo, Na filimbi yangu kuwa sauti yao waliao.

Top |  |  Next Chapter |  | Index |  | Home
Full online version here [with search engine, multilingual display and audio Bible]