Ayubu
1 Je! Waweza wewe kumvua mamba kwa ndoana? Au, kuufunga ulimi wake kwa kamba?
2 Je! Waweza kutia kamba puani mwake? Au kutoboa taya yake kwa kulabu?
3 Je! Atakusihi sana? Au, atakuambia maneno ya upole?
4 Je! Atafanya agano pamoja nawe, Umtwae kuwa mtumishi wako milele?
5 Je! Utamchezea kama ndege? Au, kumfunga kwa ajili ya wasichana wako?
6 Je! Vikosi vya wavuvi watamfanyia biashara? Watamgawanya kati ya wafanyao biashara?
7 Je! Waweza kuijaza ngozi yake na vyuma vyenye ncha, Au kichwa chake kwa vyusa?
8 Mwekee mkono wako; Vikumbuke vile vita, wala usifanye tena.
9 Tazama, kumtamani ni bure; Je! Hatambwaga chini huyo atakayemtazama?
10 Hapana aliye mkali hata akathubutu kumwamsha; Bali ni nani awezaye kusimama mbele yangu mimi?
11 Ni nani aliyetangulia kunipa hata nimlipe? Kila kilicho chini ya mbingu nzima ni changu.
12 Sitanyamaa kusema habari za via vyake, Wala nguvu zake kuu, wala umbo lake zuri.
13 Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu?
14 Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake.
15 Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri.
16 Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati.
17 Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa.
18 Kwa kuchemua kwake mwanga humemetuka, Na macho yake yanafanana na makope ya alfajiri.
19 Mienge iwakayo hutoka kinywani mwake, Na macheche ya moto huruka nje.
20 Moshi hutoka katika mianzi ya pua yake, Kama nyungu ikitokota, na manyasi yawakayo.
21 Pumzi zake huwasha makaa, Na miali ya moto hutoka kinywani mwake.
22 Katika shingo yake hukaa nguvu, Na utisho hucheza mbele yake.
23 Manofu ya nyama yake hushikamana; Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa.
24 Moyo wake una imara kama jiwe; Naam, imara kama jiwe la chini la kusagia.
25 Anapojiinua, mashujaa huogopa; Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo.
26 Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii; Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha.
27 Yeye huona chuma kuwa kama nyasi, Na shaba kama mti uliooza.
28 Mshale hauwezi kumkimbiza; Na mawe ya teo kwake hugeuka kuwa kama makapi.
29 Marungu huhesabiwa kama mabua; Naye hucheka mshindo wa mkuki ukitupwa.
30 Pande zake za chini ni kama vigae vikali; Hutandika malazi kama kuweka chombo cha kupuria nafaka juu ya matope.
31 Yeye huchemsha kilindi mfano wa nyungu; Hufanya bahari kuwa kama mafuta.
32 Hufanya mapito yake kung'aa nyuma yake Hata mtu angedhani kilindi kina mvi.
33 Juu ya nchi hapana aliyefanana naye, Aliyeumbwa pasipo oga.
34 Yeye hutazama kila kitu kilicho juu; Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.