Home |  | Audio |  | Index |  | Verses

Mithali

Chapter: 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31

1 Usiwahusudu watu waovu, Wala usitamani kuwa pamoja nao;
2 Kwa maana moyo wao hufikiri dhuluma, Na midomo yao huongea madhara.
3 Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika,
4 Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.
5 Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo;
6 Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu.
7 Kwa mpumbavu hekima haipatikani; Hafumbui kinywa chake langoni.
8 Mtu afikiriye kutenda maovu, Watu watamwita mtundu;
9 Fikira za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu.
10 Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.
11 Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.
12 Ukisema, Sisi hatukujua hayo; Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye? Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye? Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?
13 Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo.
14 Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako; Ikiwa umekwisha kuiona; Ndipo itakapofuata thawabu; Wala tumaini lako halitabatilika.
15 Ewe mtu mbaya, usiyavizie makao yake mwenye haki; Wala usipaharibu mahali pake pa kupumzika;
16 Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.
17 Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;
18 Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake.
19 Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya; Wala usiwahusudu wabaya;
20 Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika.
21 Mwanangu, mche Bwana, na mfalme; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;
22 Maana msiba wao utatokea kwa ghafula; Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao.
23 Haya nayo pia ni maneno ya wenye akili. Kupendelea watu katika hukumu si kwema.
24 Amwambiaye mtu mwovu, Wewe una haki; Kabila za watu watamlaani, taifa watamchukia.
25 Bali kwao wakemeao furaha itakuwako; Na baraka ya kufanikiwa itawajilia.
26 Aibusu midomo atoaye jawabu la haki.
27 Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.
28 Usimshuhudie jirani yako pasipo sababu, Wala usidanganye kwa midomo yako.
29 Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake.
30 Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.
31 Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.
32 Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.
33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!
34 Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.

Top |  |  Next Chapter |  | Index |  | Home
Full online version here [with search engine, multilingual display and audio Bible]