Mithali
1 Mwanangu, sikiliza hekima yangu; Tega sikio lako, mzisikie akili zangu;
2 Upate kuilinda busara, Na midomo yako iyahifadhi maarifa.
3 Maana midomo ya malaya hudondoza asali, Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
4 Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; Ni mkali kama upanga wa makali kuwili.
5 Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake zinashikamana na kuzimu;
6 Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; Njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari.
7 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Wala msiache maneno ya kinywa changu.
8 Itenge njia yako mbali naye, Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.
9 Usije ukawapa wengine heshima yako, Na wakorofi miaka yako;
10 Wageni wasije wakashiba nguvu zako; Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni;
11 Nawe ukaziombolea siku zako za mwisho, Nyama yako na mwili wako utakapoangamia;
12 Ukasema, Jinsi nilivyochukia maonyo, Na moyo wangu ukadharau kukemewa;
13 Wala sikuisikia sauti ya waalimu wangu, Wala sikuwategea sikio langu walionifundisha!
14 Nalikuwa karibu na kuingia katika maovu yote, Katikati ya mkutano na kusanyiko.
15 Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako.
16 Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu?
17 Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe.
18 Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako.
19 Ni ayala apendaye na paa apendezaye; Maziwa yake yakutoshe sikuzote; Na kwa upendo wake ushangilie daima.
20 Mwanangu! Mbona unashangilia malaya, Na kukikumbatia kifua cha mgeni?
21 Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana, Na mienendo yake yote huitafakari.
22 Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake.
23 Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, Naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake.